KISWAHILI
NA SANAA – MZIMU WA SHAABAN ROBERT.
Imetayarishwa
na Abdul Rutona.
Kwa
mujibu wa “Kamusi ya Kiswahili Sanifu”, Toleo la Pili: Lugha ni mpangilio wa
sauti na maneno unaoleta maana ambao hutumiwa na watu wa taifa au kundi fulani
kwa ajili ya kuwasiliana. Katika Makala yenye kichwa cha “Matumizi ya Lugha ya Kiswahili Katika Kazi za Sanaa”
iliyoandikwa na Bwana Khadil
Kantangayo katika Blogu yake Tarehe 13, Aprili ya mwaka 2011, Mwandishi
anaelezea kuwa lugha
ni mfumo maalumu wa sauti nasibu za kusemwa unaotumika na jamii ya utamaduni
fulani kwa ajili ya mawasiliano au kupashana habari. Anaendelea kuwa lugha zote duniani zina tabia zinazofanana
ingawa sababu hiyo haifanyi lugha zote kufanana japokuwa kuna zinazokaribiana.
Anaongezea kuwa lugha huathiriwa na lugha nyingine, na kuwa lugha huweza kuongeza msamiati na mara
nyingine huweza kufifisha msamiati na ukatoweka katika matumizi. Anamalizia kwa
kusema kuwa hakuna lugha bora kuliko
nyingine, kila lugha ni bora kwa kuwa inakidhi haja ya mawasiliano.
Ninaungana na wale
waaminio kuwa mafanikio makubwa yanayopatikana katika ujenzi wa utamaduni na
utambulisho wa nchi yoyote ni lugha. Kwa Mtanzania, lugha hiyo ni
Kiswahili…ambayo imetuunganisha wote na kutupa sifa moja muhimu ya UTAIFA.
Mwandishi
hakuishia hapo, anajaribu kuelezea Sanaa kwa ufupi kuwa Sanaa ni
ufundi wa kuwasilisha hisia na mawazo ya binadamu kwa mdomo, maandishi, michoro
na uchongaji. Anaelezea sanaa ya
maandishi kwamba imegawanyika katika tanzu kuu tatu ambazo ni Tamthiliya, Riwaya
na Ushairi na kwamba tanzu hizo zina vipengele vidogovidogo. Sanaa ya uchoraji,
Sanaa ya uchongaji na Sanaa ya Jukwaani
na kwamba Sanaa za jukwaani ni sanaa ambazo hujumuisha nyimbo za miziki,
maigizo na ngoma za kienyeji na kusisitiza kuwa
lengo likiwa ni kufikisha ujumbe kwa jamii.
Kwa
upande wangu, nitajaribu kuelezea kwa ufupi sanaa hiyo ya jukwaani hasa katika
nyimbo inavyoweza kutumika kufikisha ujumbe kwa kutumia Kiswahili. Nitatumia Santuri
ya “Mzimu wa Shaaban Robert” ya Msanii “NASH EMCEE” ambayo ni moja kati ya dira
makini zenye kila aina ya uono na fikra pevu katika kukuza na kuendeleza
utamaduni wa lugha yetu aushi ya Kiswahili. Santuri hii inakusanya vibao 18,
japo ni ina muda wa miaka kadhaa tangu ilipoanza kuuzwa, ujumbe upatikanao humo
ni endelevu.
Nitajaribu kuelezea
kwa kifupi kibao ambacho ni namba moja katika mpangilio wa vibao hivyo 18.
Kibao hicho kinaitwa “MZIMU WA SHAABAN ROBERT”. Kibao hichi kilitayarishwa na
Mtayarishaji “ABBY” pale “Tattoo records”.
Msanii kwa kuwa ni mwanaharakati wa lugha ya
Kiswahili alitumia sanaa ya kujiita Mzimu wa Shaaban Robert kuelezea historia
ya mmoja kati wa washairi bora kabisa
kupata kutokea barani Afrika. Msanii anaanza kuwaandaa waandishi kuwa wajiandae
kuandika habari za mshairi huyo aliyezaliwa Tarehe 1 Januari 1909 kijiji cha “VIBAMBANI” jirani na “MACHUI” kilomita 10
kusini mwa mji wa “Tanga” na kwamba alipata elimu yake katika Shule ya Msimbazi, jijini Dar-es-salaam kati ya miaka 1922 na 1926
alifaulu na kupata cheti cha kuridhisha na baadae kufanya kazi kwenye Mji wa “Pangani” (Aliajiriwa na serikali ya
kikoloni kama karani katika idara ya forodha huko mwaka 1926 – 1944. Bila shaka kukaa kwake
miaka mingi katika mji wa kihistoria uliokuwa mahali pa utamaduni wa Kiswahili
tena mahali patulivu kulisaidia maendeleo yake Shaaban kama mwandishi wa
Kiswahili.).
Msanii anaendelea
kumwelezea Mshairi Shaaban Robert kwamba alifanikiwa kuandika vitabu ishirini
na mbili. Baadhi ya vitabu ni: Adili na Nduguze, Kusadikika, Kufikirika, Wasifu wa Siti Binti Saad, Baada ya Miaka Hamsini, na Maisha Yangu.
Vitabu vyake vimetafsiriwa katika lugha za Kichina,
Kiingereza na Kirusi na
kuwa alifariki huko Tanga Tarehe ya 22
Juni 1962, na akazikwa huko Machui.
Kwa mambo makubwa aliyowahi
kufanya katika maisha yake, alitunza kwa zawadi ya waandishi inayoitwa
‘Margaret Wrong Memorial Prize’na pia
aliwahi-tunzwa nishani ya M.B.E. Hakika alikuwa ni BABA WA KISWAHILI.
Msanii amejitahidi
kutumia lugha ya Kiswahili katika vibao vyote 18 bila kuchanganya na lugha za
kigeni hasa Kiingereza (labda kwenye maneno machache aliyolazimika kuyatumia na
ni yale maneno yanayotumika sana amabayo hata mtaani nirahisi kueleweka). Natoa
kongole katika hili..
Kwako NASH EMCEE, Kwa
Baraka na dua zote, naamini utaendelea kufanikiwa katika kukuza na kuendeleza
lugha yetu ya Kiswahili.
#
Fikra_sahihi_huja_kwa_lugha_ya_asili.
No comments:
Post a Comment