Pages

NASH MC.

Tuesday, April 21, 2015

HAKIKA "BAADA YA CHUO" HUAKISI MAISHA YA WASOMI WENGI.

Amani iwe kwenu mashabiki wakweli wa Nash Mc, leo kutoka katika maktaba yetu tumewaletea kile tukiaminicho kuwa Hiphop ni utamaduni ugusao maisha ya mwanadamu na ulikuja kumtetea au kumsemea shida zake ila pia  katika kipengele cha kazi ya fasihi (muziki) utamaduni huu bila huwa ni akiso la jamii.

Naam ni sahihi, ila mzuka unapanda pale tu kinapomaliza kibao nambari tatu (03) katika santuri kali ya MCHOCHEZI kilichotayarishwa na TROO akiwa ni miongoni mwa watayarishaji mahiri wa muziki (Hiphop), oi, baada ya kibao hicho kibao nambari 04 kinaingia kikiwa na jina la BAADA YA CHUO nacho kimetayarishwa na TROO naamua kukisikiliza kwa makini ndipo nikagundua " "HAKIKA BAADA YA CHUO HUAKISI MAISHA WA WASOMI WENGI".

Kwani ni pale tu mshairi (Nash Mc) anapojaribu gusia hisia, mawazo na maisha halisi ya wasomi nchini Tanzania pengine na kwingineko duniani, akielezea maisha ya wasomi waliopo vyuoni na wale waliopo mtaani wakiwa hawana ajira na changamoto za maisha wazipatazo, embu ona.

Ubeti wa kwanza:
Unaelezea mwanzo wa masomo kwa wanafunzi wa vyuo ukihusisha suala la fedha kwa ajili ya kujikumu (boom) hasa kwa wale wenye nayo wasiokuwanayo hivyo kupelekea baadhi yao "kula mara moja kwa siku"  kwani hawakuwa na kitu hasa boom lilipochelewa, hivyo kupelekea watoto wa kike kujiuza kila kona ili wapate pesa ya kutumia ndipo hapo sasa "ukistahajabu ya mimba utayaona ya ngoma".

Pia kutokana na kukosa fedha hivyo mawazo kuwafanya wanafunzi wengi wafeli masomo yao (kupata sup) na kuwataka warudi mapema vyuoni kurekebisha, lakini wapo waliodisco kabisa. Ingawa wanapitia hali zote hizo hatimaye msanii anawaambia.

... Sasa umemaliza chuo karibu nyumbani,
 Wenzio mwaka wa tano bado tupo maskani,
Tuna shahada mbili moja ya darasani,
Ya pili ya mtaani tunaishi kwa imani,
Tumedharaulika mpaka tumezoea,
Hatujapata kazi na umri unasogea,
Kumbuka elimu ya huku darasa ndiyo mtaa,
Wahadhiri walimwengu hakuna chakushanga,
Ukiwavunjia heshima haraka unageuzwa chengu,
Mtaa una elimu kubwa zaidi ya kule chuoni uliposoma,
Kwakuwa umesharudi  mwenyewe utayaona/

Ndiyo, ndiyo hii ni Hiphop iakisiyo jamii kwani katika jamii zetu sisi wenyewe tumekuwa mashuhuda wa hiki ambacho msanii amekighani katika kemo zake mahiri kabisa ila sasa uhondo unapatikana zaidi katika ubeti wa pili ambapo msanii anazungumzia maneno ya walimwengu kwa wale waliohitimu na wamerudi mtaani pamoja na harakati zao za kutafuta kazi na changamoto zingine nyingi.

Ubeti wa pili: 
Dharau na kejeli watu watakuponda,
Yule hana kazi kafeli kashaboronga,
Hawajaona vyeti vyako lakini bado watachonga,
Hao ndio waliomwengu usipowajua mawazo yatakuzonga,
Utajikuta unakonda unapaswa kujifunza wala usipagawe,
Mti wenye matunda ndo hupigwa mawe,
Fanya utakalofanya kwao hakuna la maana,
Zaidi ya kuonekana unajifanya msomi.
Wengine chuki zao wameziweka rohoni,
Wanasubiri wakosee wakutemee poo mate usoni,
Poleni wanazuoni,
Unaomba sana kazi kila siku unadunda,
Kaka hauna mavumba, 
Wewe na vyeti vyako ofisi zote za mjini umeshavuruga,
Kila fomu ya maombi imeandikwa kwenye mabano,
Mwombaji awe na sifa ya uzoefu (uzoefu gani) wa miaka mitano,
Ndo namaliza chuo naupata wapi uzoefu kwa mfano,
Kampuni kibao C.V umeshapeleka zikaeleweka,
Lakini mpaka leo hujaitwa kwenye usahili kisa hauna refa,
Rushwa ya ngono ndo hapo inaingia dada zangu wanaachia,
Mtoto wakiume unacho cha kutumia au ndo uchumi unao halafu unaukalia,
Mawazo ya kurogwa pia yatakujia, inabdi kuvumilia,
Usikate tamaa kitivo cha mtaa ndo hiki unapitia,
Na hizi ndo elimu ambazo nilikwambia,
Maisha baada ya chuo unaweza ukajifukia/.

Kwa ufasaha kabisa msanii anaifikishia jamii yake changamoto zinazowakabili kila siku katika jamii zao hasa ukosefu wa ajira na mwishoni anawapa ushauri, na kwa uwazi kabisa katika jicho la kichambuzi utagundua yote haya yanatokana na umasikini katika jamii zetu, uongozi mbovu n.k, hivyo kupitia wimbo huu jamii inabidi ipambane kujiletea maendeleo yake kwa kufa na kupona.

Mishororo ya ubeti huu wa mwisho umejawa ukweli mtupu (unahakisi) wa maisha ya wanafunzi wengi wa vyuo na maisha yao pindi wafikapo mtaani baada ya kuhitumu, ingawa hukutana na changamoto nyingi na nyingine zisizovumilika msanii (Nash Mc) anawapa moyo na ushauri kuwa "watu kusema ni kazi yao ... na waungwana husema namwachia Mungu, hivyo yote hayo wamwachie Muumba wa mbingu na ardhi (Mungu).

Angalia: Kibao nambari 04.






+255 (0) 654 30 40 30, Mwanazuoni (Mhariri andiko).
 






7 comments: