Pages

Thursday, February 20, 2014

" NAANDIKA ", NI KIBAO KIPYA CHA HIPHOP MWANZONI MWA 2014, JE WAJUA KIMEBEBA MAUDHUI YAPI?, FUATILIA HAPA UJIFUNZE.

NASH MC kwanini kaandika, na kuna nini kwenye "NAANDIKA"?.
Salamu kwanza kwa kila mmoja, naam!, naimani kila mmoja yu salama, na anaendelea vyema na shughuli za ujenzi taifa, na kwa wasio vyema kiafya na mengine Mola awape shifaa katika hilo.
HIPHOP, ndiyo kitu nachogusia hapa kwa maana ya wasanii wake (watu waishio ndaniye), au jamii nzima, lakini mguso wangu ulipewa nguvu zaidi pale nilipotumiwa wimbo huu "NAANDIKA" na leo nilipoupakua ili nipate ukiwa na kiwango bora zaidi (high quality mp3) kwa maana wakwanza ulitumwa kwa whatsapp.
Lakini pia kama ilivyo ada huwa na kitabia cha kupitia hapa na pale hili kupata kiduchu kuhusu utamaduni huu wa hiphop au sanaa kwa ujumla hivyo safari yangu ikapitia hapa, Hanzi, M.S, (2012), Chuo Kikuu cha HipHop, Ubunifu Wetu Printing Press, Dar es Salaam: Tanzania, katika kurasa kama nambari 15, na nyingine kadhaa, ndipo nkagundua kuwa mwandishi kakumbusha kuwa HIPHOP NI MAARIFA, pia aligusia nguzo za hiphop hapo miye nkajikita elewa maarifa kama nguzo ya utamaduni huu.
Yote hayo, nkaja yaweka katika uchambuzi huu wa wimbo "NAANDIKA", toka kwa NASH MC, kama msanii wa HIPHOP niligundua kuwa katika NGUZO YA MAARIFA imesawiriwa vyema naye, kwani MWANAHIPHOP yoyote anakumbushwa kufuatilia mengi katika jamii, kusoma ili aweze kuwa na uelewa mpana yaani asiwe nyuma (ajisasishe).
Hivyo sasa, Nash Mc katika kibao hiki kupitia ghani zake kaongelea mengi yatokeayo duniani (jamii), ambayo pengine ukiyasikiza vyema waweza pata jambo na kugundua vitu vitakavyoleta mabadiliko, wimbo huu kwa upande wa fani msanii ameonesha falsafa yake ambayo ni mapinduzi katika fikra za wengi jamiini kwa mtindo ninaoweza uita ghani yenye mlengo kumbushi,ambayo imechokoa mambo bila kutoa masuluhisho ya jumla, kwa maudhui kuna pipa la dhamira ambacho ndiyo lengo la maandishi haya.
Msanii anaonesha haya yafuatayo. 1. Suala la imani (ya kidini), kuwa yeye kama msanii anapaswa/ anaandika kuhusu utukufu wa Mungu wake, ambaye ndiye anamuongoza kwenye maisha yake, na si mwingine yeyote, hivyo hili ni kama kumbusho kwa wanajamii wamuamiao Mungu kumkumbuka na kumtukuza (hasa wasanii), wasiandike raha tu (starehe) na kumsahau yeye, rejea ubeti wa kwanza anaposema "naandika kuhusu utukufu wa mungu wangu, anayeniongoza kwenye haya maisha yangu/''.
2.Suala la mapenzi ya dhati ya utamaduni. Msanii nash Mc anaonekana ni mtu mwenye mapenzi ya dhati ya utamaduni wa HIPHOP na abadani hakubali utamaduni huu upotee kizembe kwa kupotoshwa, hili laonekana pale aliposema "bila kusahau utamaduni wa HIPHOP naipenda hii kitu, hivyo sasa kuacha jambo kwa wapenzi wa utamaduni huu kuupenda vilivyo utamaduni huu kwa kuunga mkono harakati, kazi za wasanii wake.
Pia msanii anaendelea dodosa mengi zaidi pale anapoonesha yatokeayo Afrika na nyumbani pia (Tanzania), mfano. 3.Suala la vita vya wenyewe kwa wenyewe (Afrika ya Kati, Kongo na Sudan). Kweli kakumbusha jambo adhimu linalopaswa kuandikwa na Wasanii hasa wa HIPHOP ambao ndio utamaduni KOMBOZI WA JAMII, na kuacha kuandika kuhusu bifu, katika hili msanii anaonesha athari za vita hivyo kama mauaji ya akina mama na watoto, udhalilishaji wa wanadamu, ikiwa ni athari ya vita, msanii kakumbusha kuwa "naandika", kama kichokoo cha kila mwanahiphop kugusia haya, naandika kuhusu.
4.Kupanda kwa gharama za maji na umeme. Kwa watu wa majumbani ambao ndiyo wengi nchini Tanzania wenye kipato cha chini na maisha yao ni magumu hivyo hili ni kama gharika (TSUNAMI), hapa anakumbusha serikali iliangalie hili kwani ni mwimba kwa jamii hiyo yenye hali chini.(rejea kibao hiko).
5.Suala la kukosa uzalendo, dili za magendo, uuzaji wa pembe ze tembo. Yote haya mwandishi ANAANDIKA na kujaribu chokoza hisia za wasikilizaji wake pengine kuwafumbua macho kuhusu hali ilivyo nchini kwetu pengine Afrika, ambapo wananchi na viongozi wanakosa uzalendo juu ya mali zao, pengine ndipo panapopelekea dili za magendo na mauaji ya tembo kwa watu wachache na kuhujumu rasirimali taifa.
6.Kutokuwepo na mgawanyo sahihi wa keki ya taifa (utabaka)/ faida-rasirimali. Hapa navuta hisia zangu katika haya yatokeayo Afrika hasa huko Kongo, Afrika ya Kati, Sudan ambapo mapigano yao kwa asilimia kadhaa chanzo chake ni rasilimali zilizopo, lkn pia tukumbuke yale yaliyotokea Mtwara (sakata la gesi), je vipi kuhusu ule mgogoro wa ardhi (wafugaji na wakulima) huko Morogoro, ndipo msanii akasema "naandika" kuhusu gesi, mbuga, ardhi na madini kama vitu muhimu ambavyo mara nyingi siku hizi wanapewa watu wenye mifuko mizito (wawekezaji) na kuacha wazawa wakilia na kunyanyasika, (rejea maeneo yenye migodi na athari zake).
7.Suala la kupotea kwa vijana katika mitaa (wavulana kwa wasichana). Ambao ndiyo nguvu kazi kwa jamii, mfano.pale anapoghani " njoo kwenye mitaa vijana wamepotea vibaya, dada zetu wamekuwa malaya/", kwa msongo wa mawazo wanatenda mabaya/, mpaka wanasahau kuhusu dhambi wao pombe na khaya, hivyo mwandishi anagusia kuhusu kuacha hayo mambo maana ni hatari., kwakweli NAANDIKA imeonesha mengi embu ona haya pia. 8.Athari za ngono isiyo salama, inayomaliza kundi kubwa la vijana. 9.Wasanii kutotunga kazi zinazohamasisha ngono za jinsia moja, na kumkumbusha Rais kuwa akitia sahihi yeye ni muoga (kwa kutokuwa na msimamo wake), hivyo asikubali mashinikizo ya mataifa ya magharibi.
10.Kutokubadilika kifasalfa (kama msanii), kwa minajiri ya kupata muda wa kusikika hewani ili upate mafanikio ilhali unaandika vitu visomaana katika jamii mfano. kuwepo kwa ghala kubwa la nyimbo za mapenzi kila kukicha wakati jamii ina mambo mengi ya kuzungumzia mf. anasema " Unaandika kuhusu mapenzi hiyo ni kwa hisani ya radio fulani, jambo ambalo linawarudisha wasanii utumwani (kwa kuwanyenyekea watangazaji, wadundishaji wapige kazi zao), Pia anasisitiza.
11.Matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye fani ya ushairi. Kama muega mmoja wapo wa uzalendo na kufanya kazi zetu zikubalike mbali kwa kupenda vyetu, na kuacha ule utumwa kuwa ukighani au imba kingereza ndiyo mjuvi sana, hivyo kuonesha kuwa huo ni ubunifu tu katika lugha japo si lazima sana, kwani msanii anaamini " kuwa fikra sahihi huja kwa lugha asili" nayo ni Kiswahili.
12.Kutobadilika kutoka kule ulikokuwa (HIPHOP), na kwenda katika baibuda kiduku, kwaito kisa mafanikio ya haraka, hii si sawa kwa mwana hiphop halisi, kwani jamii inatakiwa ifahamu kuwa "nakala mia moja za HIPHOP ni bora kuliko nakala 1000 za muziki mwingine, usiozungumzia jamii na ukweli (ukombozi).
13.Kuwepo kwa watangazaji na wadundishaji wala rushwa. Msanii anawakumbusha hao kuwa "wasiombe kukutwa na takukuru ya mtaa.
Kwa ujumla msanii NASH MC kazungumzia mengi katika kibao hiki katika aina ya ghani ya kunata juu ya mdundo mahiri, katika mtindo wa kukumbusha jamii, juu ya mambo mbalimbali yanayoikabili, na kuwachokoa wasanii wengine wa Hip Hop "waandike" juu ya haya aliyoyandondoa kibaoni humo, naam!!, haya ndiyo maarifa na hii ndiyo nguzo mhimili katika hiphop, utamaduni adhimu kabisa, tafuta kibao hiko ujikumbushe mengi.
Mwanazuoni, 0654 30 40 30.

No comments:

Post a Comment