Pages

Friday, May 1, 2015

KISWAHILI NA SANAA – MZIMU WA SHAABAN ROBERT.



KISWAHILI NA SANAA – MZIMU WA SHAABAN ROBERT.

Imetayarishwa na Abdul Rutona.

Kwa mujibu wa “Kamusi ya Kiswahili Sanifu”, Toleo la Pili: Lugha ni mpangilio wa sauti na maneno unaoleta maana ambao hutumiwa na watu wa taifa au kundi fulani kwa ajili ya kuwasiliana. Katika Makala yenye kichwa cha “Matumizi ya Lugha ya Kiswahili Katika Kazi za Sanaa” iliyoandikwa na Bwana  Khadil Kantangayo katika Blogu yake Tarehe 13, Aprili ya mwaka 2011, Mwandishi anaelezea kuwa  lugha ni mfumo maalumu wa sauti nasibu za kusemwa unaotumika na jamii ya utamaduni fulani kwa ajili ya mawasiliano au kupashana habari. Anaendelea kuwa  lugha zote duniani zina tabia zinazofanana ingawa sababu hiyo haifanyi lugha zote kufanana japokuwa kuna zinazokaribiana. Anaongezea kuwa lugha huathiriwa na lugha nyingine, na kuwa  lugha huweza kuongeza msamiati na mara nyingine huweza kufifisha msamiati na ukatoweka katika matumizi. Anamalizia kwa kusema kuwa  hakuna lugha bora kuliko nyingine, kila lugha ni bora kwa kuwa inakidhi haja ya mawasiliano.

Ninaungana na wale waaminio kuwa mafanikio makubwa yanayopatikana katika ujenzi wa utamaduni na utambulisho wa nchi yoyote ni lugha. Kwa Mtanzania, lugha hiyo ni Kiswahili…ambayo imetuunganisha wote na kutupa sifa moja muhimu ya UTAIFA.
Mwandishi hakuishia hapo, anajaribu kuelezea Sanaa kwa ufupi kuwa Sanaa ni ufundi wa kuwasilisha hisia na mawazo ya binadamu kwa mdomo, maandishi, michoro na uchongaji. Anaelezea  sanaa ya maandishi kwamba imegawanyika katika tanzu kuu tatu ambazo ni Tamthiliya, Riwaya na Ushairi na kwamba tanzu hizo zina vipengele vidogovidogo. Sanaa ya uchoraji, Sanaa ya uchongaji  na Sanaa ya Jukwaani na kwamba Sanaa za jukwaani ni sanaa ambazo hujumuisha nyimbo za miziki, maigizo na ngoma za kienyeji na kusisitiza kuwa  lengo likiwa ni kufikisha ujumbe kwa jamii.

Kwa upande wangu, nitajaribu kuelezea kwa ufupi sanaa hiyo ya jukwaani hasa katika nyimbo inavyoweza kutumika kufikisha ujumbe kwa kutumia Kiswahili. Nitatumia Santuri ya “Mzimu wa Shaaban Robert” ya Msanii “NASH EMCEE” ambayo ni moja kati ya dira makini zenye kila aina ya uono na fikra pevu katika kukuza na kuendeleza utamaduni wa lugha yetu aushi ya Kiswahili. Santuri hii inakusanya vibao 18, japo ni ina muda wa miaka kadhaa tangu ilipoanza kuuzwa, ujumbe upatikanao humo ni endelevu.


Nitajaribu kuelezea kwa kifupi kibao ambacho ni namba moja katika mpangilio wa vibao hivyo 18. Kibao hicho kinaitwa “MZIMU WA SHAABAN ROBERT”. Kibao hichi kilitayarishwa na Mtayarishaji “ABBY” pale “Tattoo records”.
Msanii kwa kuwa ni mwanaharakati wa lugha ya Kiswahili alitumia sanaa ya kujiita Mzimu wa Shaaban Robert kuelezea historia ya mmoja kati wa  washairi bora kabisa kupata kutokea barani Afrika. Msanii anaanza kuwaandaa waandishi kuwa wajiandae kuandika habari za mshairi huyo aliyezaliwa Tarehe 1 Januari 1909 kijiji cha “VIBAMBANI jirani na MACHUI kilomita 10 kusini mwa mji wa “Tanga” na kwamba alipata elimu yake katika Shule ya Msimbazi, jijini Dar-es-salaam kati ya miaka 1922 na 1926 alifaulu na kupata cheti cha kuridhisha na baadae kufanya kazi kwenye Mji wa “Pangani” (Aliajiriwa na serikali ya kikoloni kama karani katika idara ya forodha huko  mwaka 1926 – 1944. Bila shaka kukaa kwake miaka mingi katika mji wa kihistoria uliokuwa mahali pa utamaduni wa Kiswahili tena mahali patulivu kulisaidia maendeleo yake Shaaban kama mwandishi wa Kiswahili.).
Msanii anaendelea kumwelezea Mshairi Shaaban Robert kwamba alifanikiwa kuandika vitabu ishirini na mbili. Baadhi ya vitabu ni: Adili na Nduguze, Kusadikika, Kufikirika, Wasifu wa Siti Binti Saad, Baada ya Miaka Hamsini, na Maisha Yangu. Vitabu vyake vimetafsiriwa katika lugha za Kichina, Kiingereza na Kirusi na kuwa alifariki  huko Tanga Tarehe ya 22 Juni 1962, na akazikwa  huko Machui.

Kwa mambo makubwa aliyowahi kufanya katika maisha yake, alitunza kwa zawadi ya waandishi inayoitwa ‘Margaret Wrong Memorial Prize’na  pia aliwahi-tunzwa nishani ya M.B.E. Hakika alikuwa ni BABA WA KISWAHILI.
Msanii amejitahidi kutumia lugha ya Kiswahili katika vibao vyote 18 bila kuchanganya na lugha za kigeni hasa Kiingereza (labda kwenye maneno machache aliyolazimika kuyatumia na ni yale maneno yanayotumika sana amabayo hata mtaani nirahisi kueleweka). Natoa kongole katika hili..
Kwako NASH EMCEE, Kwa Baraka na dua zote, naamini utaendelea kufanikiwa katika kukuza na kuendeleza lugha yetu ya Kiswahili.

# Fikra_sahihi_huja_kwa_lugha_ya_asili.

No comments:

Post a Comment